“Unajituma sana, lakini bila maarifa na mwelekeo, utachoka bure.”
Kama wewe ni mjasiriamali unayeamka kila siku mapema kwenda sokoni, kuendesha saluni, kuuza mtandaoni, au hata kufanya kazi ya mikono tunakupongeza. Lakini pia tunakuuliza swali moja muhimu:
Biashara yako unaifanya kwa mpango au kwa kubahatisha?
Wajasiriamali wengi Tanzania wanafanya biashara kwa nguvu zote, lakini bila mpango, bila mikakati, na bila kujua kesho biashara yao itaenda wapi. Hii ndiyo tunaita “biashara kichaa” unafanya kwa mazoea tu, kwa sababu umeona wengine wanafanya, au kwa sababu umezoea.
Na ukweli ni huu:
Biashara bila maarifa ni mzigo. Biashara bila mpango ni hatari. Biashara bila utekelezaji ni ndoto isiyotimia.
Mifano ni mingi, na ya kila siku:
Mama Fatma ana kibanda cha vyakula Sinza. Kila siku anaingiza hela nzuri, lakini mwisho wa mwezi hajui hela hiyo imeishia wapi. Hana mpango wa matumizi, hana mpango wa kukuza biashara yake. Akiulizwa faida ni kiasi gani, anasema: “sijui, bora hela iingie tu.”
Elias anauza nguo mtandaoni kupitia WhatsApp. Ana bidhaa nzuri, lakini hawezi kueleza ni kwa nini mteja anapaswa kununua kwake. Hajui namna ya kutangaza vizuri, hajui jinsi ya kuweka bei ya ushindani, na hana huduma ya wateja iliyo bora. Anafanya kwa kubahatisha.
Furaha alianza kuuza sabuni baada ya kuona marafiki zake wanafanya vizuri. Lakini hakuwa na mpango. Hakujua ukubwa wa soko, hakujua aina ya wateja anaowalenga. Mwezi mmoja baadaye, alikata tamaa na akaacha.
Wote hawa ni wajasiriamali wa kweli, lakini bila maarifa, bila mwelekeo, bila mfumo wa utekelezaji biashara zao hubakia kwenye mzunguko wa kuchoka, kuchanganyikiwa, na hatimaye kuacha.
Madhara ya kuendesha biashara kwa mazoea badala ya maarifa ni makubwa kuliko unavyodhani.
Kila siku unaamka mapema, unakimbizana na muda, unahangaika kusambaza bidhaa, kufuatilia wateja, kubeba mizigo au kupika bidhaa zako. Lakini mwisho wa siku, ukiangalia mkononi hakuna faida ya kueleweka. Hali hii inakufanya uchoke si kwa sababu hujajituma, bali kwa sababu huoni matokeo ya jitihada zako. Na hiyo hupelekea mtu kukata tamaa mapema.
Kwa mfano, Fatuma anapika maandazi kila siku saa 11 alfajiri, lakini mwezi ukimalizika hana hata shilingi ya kuweka akiba au kununua vifaa vipya. Biashara inamchosha kuliko kumpa matumaini.
Unanunua bidhaa, unauza, lakini huwezi kueleza umepata faida au hasara. Hauandiki mapato wala matumizi. Hujui bei halisi ya manunuzi yako, wala hujapanga kiwango cha faida unachotaka. Mwisho wa siku unashangaa, pesa inakatika tu!
Kwa mfano, Daudi anauza juice za miwa mitaani. Kila siku anaingiza elfu 20 hadi 30. Lakini hadi mwisho wa mwezi, ana madeni kwa supplier na hajui pesa zote zimeishia wapi.
Biashara nzuri haitegemei wateja wapya kila siku. Wateja wa kudumu ndio msingi wa ukuaji. Lakini bila mpango wa huduma bora, bei zenye kueleweka, au kujua mahitaji ya mteja wako, ni vigumu kuwashikilia. Wateja wanajisikia kama hawathaminiwi na huamua kutafuta huduma bora kwingine.
Fikiria, Asha ana saluni nzuri lakini hana ratiba wala mfumo wa kuhifadhi namba za wateja. Hana huduma ya “appointment” wala mawasiliano ya mara kwa mara na wateja wake. Matokeo yake — wateja huja mara moja, kisha hawarudi tena.
Mashirika mengi, taasisi za kifedha, na hata wafadhili wa miradi wanataka kuona mpango wa biashara, mahesabu ya mapato na matumizi, au hata taarifa za mauzo. Bila taarifa hizi, hata ukipewa nafasi ya kupata msaada au mkopo, unaogopa kujaribu kwa sababu huwezi kuonyesha hali halisi ya biashara yako.
Kwa mfano, Juma aliambiwa na benki atoe projection ya faida ya miezi 6 na mpango wa matumizi. Alishindwa kabisa kwa sababu hajawahi hata kuandika mauzo ya siku moja.
Biashara yoyote ina changamoto kuna siku mauzo ni madogo, wateja hawaji, au bidhaa zinaharibika. Lakini bila mpango madhubuti, changamoto hizi zinapokuja zinakuvunja kabisa. Huna ramani ya kujua nini cha kufanya wakati mambo hayaendi sawa. Hakuna plan B. Hujui jinsi ya kupunguza hasara, au njia mbadala ya mapato.
Kwa mfano, Rehema aliwekeza kwenye kuuza vitu vya shule. Siku moja bidhaa zake zilipotea kutokana na uharibifu wa mvua. Hakuwa na akiba wala mpango wa kujipanga tena. Akaamua kuacha biashara kabisa.
Biashara yenye mpango inahitaji maarifa. Inahitaji uelewa wa soko, uelewa wa bei, mbinu za kuhudumia mteja, uwezo wa kufanya maamuzi kwa kutumia takwimu, na uthubutu wa kuwekeza kwa uelewa.
Kreative Karakana tumejitoa kusaidia wajasiriamali kuacha maisha ya kufanya biashara kwa kubahatisha na kuanza maisha ya kufanya biashara kwa maarifa. Tumetengeneza jukwaa la kozi fupi, za mtandaoni, zenye maudhui halisi ya biashara ndogondogo na za kati zinazoendana kabisa na maisha ya wajasiriamali wa Kitanzania.
Je, Umechoka Kufanya Biashara Bila Mpango?
Kama umewahi kusema “Nafanya biashara lakini sioni maendeleo…”
Kama umewahi kujiuliza “Ninapata faida kweli?”
Kama umeshawahi kukata tamaa kwa sababu biashara haieleweki…
Basi huu ndio wakati wa kubadilika.
VICOBA na Maendeleo – Jinsi ya kutumia vikundi kama chanzo salama na cha kuaminika cha mtaji.
Huduma kwa Wateja wa Biashara Ndogo – Mbinu rahisi za kuwafanya wateja wako warudi tena.
Kuweka Bei Kwa Faida – Acha kupanga bei kwa kuangalia jirani; jua hesabu zako.
Kutengeneza Chapa ya Biashara Yako – Jifunze namna ya kujitofautisha sokoni hata kama unauza bidhaa zile zile.
Biashara Mtandaoni kwa Kompyuta au Simu Yako – Uko WhatsApp au Instagram? Tumia vizuri kuuza kwa ufanisi.
Kozi hizi ni fupi, rahisi kuelewa, hazihitaji lugha ngumu, na unaweza kuzisoma hata ukiwa kwenye boda au sokoni. Kozi zinafundishwa na wajasiriamali halisi sio theory, ni uhalisia.
Drag file here or click the button.